Korea Kaskazini imedai kuwa imenasa mpango wa siri wa Marekani wakishirikiana na Korea Kusini kutaka kumuua kiongozi wao mkuu, Kim Jong-un kwa kutumia kemikali.
Vyombo vya habari vya Korea Kaskazini vimeripoti kuwa Marekani imewatumia magaidi kwa msaada wa shirika la kijasusi la CIA kuwapenyeza mawakala waliokula njama za kutaka kumuangamiza kiongozi huyo kwa kutumia bio-kemikali na mionzi maalum.
Taarifa rasmi iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Korea Kaskazini imeeleza kuwa watawasaka kwa nguvu zote mawakala hao waliotumwa na kwamba watawaangamiza bila huruma.
Hata hivyo, CIA wamekataa kutoa tamko lolote kuhusu tuhuma hizo nzito za Korea Kaskazini, kwa mujibu wa BBC.
Tuhuma hizo zimekuja wakati ambapo kumekuwa na taharuki katika rasi ya Korea, baada ya Marekani kusogeza meli zake za kivita kwa lengo la kujiandaa kuishambulia Korea Kaskazini kutokana na kukaidi azimio la kutoendelea na majaribio ya makombora ya kinyuklia.
Korea Kaskazini imekuwa ikisisitiza kuwa haitasitisha majaribio ya makombora hayo na kwamba itajibu kwa vita kamili endapo itashambuliwa kwa namna yoyote kutoka upande wowote wa dunia.
Rais wa Marekani, Donald Trump aliahidi kumaliza mpango wa Korea Kusini wa kuendeleza utengenezaji wa silaha za nyuklia, kwa njia ya mazungumzo au vinginevyo.