Joto la taharuki kati ya Marekani na Korea Kaskazini limeendelea kupanda kuhusu makombora ya kinyuklia, baada ya Korea kudaiwa kujipanga kufyatua kombora jingine kama sehemu ya jaribio la mashine zake mpya za kurusha makombora hayo.
Taarifa za jaribio hilo zimetolewa na maafisa wa Marekani ambao wamedai kuwa hilo litakuwa jaribio la kwanza kubwa zaidi kufanywa na Korea Kaskazini tangu mwezi Machi mwaka huu.
Rais Trump tayari alishatahadharisha kuhusu mpango huo wa Korea Kaskazini, akieleza kuwa hatawavumilia.
Hata hivyo, Korea Kaskazini imeendelea kusisitiza kuwa haitaacha kufanya majaribio yake ya makombora huku ikidai makombora yake yanaweza kufika katika kona nyingi za dunia ikiwa ni pamoja na Marekani.
Kwa mujibu wa BBC, shirika la ujasusi la Marekani limeeleza kuwa mpango wa makombora ya kinyuklia ya Korea Kaskazini unakaribia kufanikiwa.