Korea Kaskazini imeapa kulipiza kisasi na kuhakikisha kuwa Marekani imelipia gharama zote zitakazo sababishwa na vikwazo vilivyowekwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya mpango wake wa silaha za nyuklia.
Shirika la habari la Korea Kaskazini (KCNA) limesema kuwa vikwazo vilivyowekwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, vinatokana na ushawishi mkubwa wa Marekani kitu ilicho kiita ni ukiukwaji wa uhuru wa nchi katika kufanya shughuli zake za kujilinda na za kimaendeleo.
Aidha, majirani zao Korea Kusini imesema kuwa Korea Kaskazini imekataa ombi la kufanya mazungumzo ya kidiplomasia ili waweze kutatua mgogoro huo uliosababisha kuwekewa vikwazo vya kiuchumi.
Vikwazo ilivyowekewa Korea Kaskazini vimelenga kuzuia mauzo ya bidhaa za nchi hiyo kwa theluthi moja, ambapo imeituhumu Marekani kuwa ni chanzo cha vikwazo hivyo ambavyo vimelenga kudhoofisha mpango wake wa nyuklia.
Hata hivyo, Korea ya Kaskazini imesema kuwa pamoja na kuwekewa vikwazo hivyo, kamwe haitachana na mpango wake huo wa kutengeneza silaha za masafa marefu na zile za nyuklia