Korea Kaskazini imesema kuwa inatafakari uwezekano wa kurusha makombora karibu na jimbo la Marekani la Guam katika bahari ya Pasifiki, muda mfupi mara baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutishia kushambulia mji mkuu wa nchi hiyo Pyongyang.

Shirika la habari la Serikali ya Korea Kaskazini limesema kuwa taifa hilo linatafakari mpango huo wa kurusha makombora ya masafa ya kati na marefu karibu na Guam, eneo ambalo ni kituo cha Marekani cha kutungua makombora.

Aidha, taarifa hiyo inaashiria kuongezeka kwa uhasama kati ya nchi hizo mbili, mara baada ya Umoja wa Mataifa hivi karibuni kuiwekea vikwazo vya kiuchumi Korea Kaskazini ambayo imeituhumu Marekani kuhusika katika suala hilo.

Kwa upande wake, Rais wa Marekani, Donald Trump amesema kuwa Korea Kaskazini imefikia kiwango cha hali ya juu cha utengenezaji wa silaha za nyuklia kitu ambacho imesema ni tishio kwa usalama wa dunia.

Hata hivyo, mgogoro huo kati ya Marekani na Korea Kaskazini umezidi mara baada ya Pyongyang kufanyia majaribio ya makombora mawili yenye uwezo wa kusafiri kutoka bara moja hadi nyingine, na kudai kuwa sasa ina makombora yanayoweza kufika moja kwa moja mpaka Marekani bara.

 

Hizi Ndio Sababu Za Ngassa Kukwama Kwenye Usajili Wa Young Africans
Shaffih Dauda Atengua Kauli, Arejea Kundini