Korea Kaskazini imeanza kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano kati ya Rais Donald Trump na kiongozi wao, Kim Jong-un kwa kurejesha mabaki ya wanajeshi wa Marekani waliokufa kwenye ardhi ya nchi hiyo.
Nchi hiyo imeripotiwa kukabidhi kwa jeshi la Marekani mabaki ya maelfu ya waliokuwa wapiganaji wa Marekani waliokufa kwenye vita kati ya Korea Kaskazini na Korea Kusini, mwaka 1950-1953.
Ndege ya jeshi la Marekani imefanya safari kadhaa kwenye Pwani ya Korea Kaskazini na kubeba mabaki hayo ambayo yamepelekwa nchini Korea Kusini.
Kim Jong-un alimuahidi Trump kuwa atakabidhi mabaki hayo walipokutana nchini Singapore; na hii imekuwa ahadi ya kwanza inayoonekana kutekelezwa kwa kiwango cha asilimia 100.
Ikulu ya Marekani imeelezwa kufurahishwa na hatua hiyo ya Korea Kaskazini.
“Leo Kim Jong-un ametekeleza sehemu ya ahadi yake aliyompa Rais Trump kurejesha mabaki ya wapiganaji wetu. Tumetiwa moyo na hatua iliyochukuliwa na Korea Kaskazini kwa ajili ya mabadiliko chanya,” imeeleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa ratiba, Agosti 1 mwaka huu wanajeshi wa Marekani watatoa heshima zao kwa mabaki ya wapiganaji hao katika eneo la kijeshi la Osan nchini Korea Kusini.
Takribani wanajeshi 7,700 wa Marekani wanatajwa kupoteza maisha kwenye vita ya Korea Kaskazini na Korea Kusini, katika miaka ya 1950.
Mabaki ya askari 5,300 wa Marekani yalikuwa kwenye ardhi ya Korea Kaskazini.
Katika vita hiyo mbaya kuwahi kutokea kwenye eneo hilo, mamilioni ya watu walipoteza maisha ikiwa ni pamoja na wanajeshi 36,000 wa Marekani.