Korea Kaskazini imetishia kutumia mabomu ya nyuklia kuizamisha Japan na kuigeuza Marekani kuwa mavumbi ikiwa ni hatua ya kujibu vikwazo vipya ilivyowekewa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, tamko la Korea Kaskazini lililotolewa kwa vyombo vya habari limeeleza kuwa Japan haitakiwi kuonekana tena.
“Visiwa vinne vya archipelago (vilivyogawanyika kimakundi) vinapaswa kuzamishwa baharini kwa mabomu ya nyuklia ya Juche. Japan haipaswi kamwe kuwa karibu na sisi. Na tuipunguze ardhi kavu ya Marekani kuwa mavumbi na kiza” Reuters wanalikariri tamko hilo.
Katika hatua nyingine, tamko hilo linadaiwa kuushambulia Umoja wa Mataifa kwa madai kuwa ni chombo kiovu kinachofanya kazi kwa maslahi ya Marekani.
Katibu Mkuu Kiongozi wa Baraza la Mawaziri la Japan, Yoshihinde Suga alilaani tamko hilo alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari jana. Suga alisema kuwa tamko hilo la vitisho halikubaliki na kwamba linaongeza taharuki ya kiusalama katika ukanda huo.
Hata hivyo, China imetoa tamko lake ikiitaka Marekani kufanya maamuzi sahihi ya kidiplomasia na kisiasa haraka iwezekanavyo na kutafuta namna ya kupata suluhisho la mgogoro huo kwa njia ya amani.
Marekani imekuwa ikiishutumu Korea Kaskazini kwa kukiuka sheria za Kimataifa na kufanya majaribio ya mabomu ya nyuklia.