Kozi ya Grassroots kwa Vijana kuanzia miaka 6-12, itafanyika mkoani Mbeya kuanzia Novemba 27, 2017 mpaka Desemba 1, mwaka huu.

Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Salum Madadi amesema kozi hiyo itahusisha walimu wa Shule za Msingi za mikoa ya Songwe, Katavi, Rukwa na wenyeji Mbeya.

Jumla ya washiriki 30 watahudhuria kozi hiyo ambapo kila mkoa utatoa washiriki saba (7) isipokuwa wenyeji Mbeya ambao watatoa washiriki tisa (9).

Kozi hiyo imezingatia jenda kwa kila mkoa unatakiwa kutoa idadi sawa au Wanawake wawe wengi zaidi ya Wanaume ili kutoa hamasa zaidi kwa Wanawake kujifunza.

Kozi hiyo ya Grassroots itakwenda sambamba na Kampeni ya ‘Live Your Goal’ ikiwa na maana ya ‘Ishi ndoto zako’ itayofanyika Novemba 29, 2017 ikiwa na lengo la kutoa hamasa kwa soka la Wanawake.

Kampeni hiyo ya Live Your Goal inalenga kutoa hamasa kwa wadau waujue, waupende na kuheshimu soka la Wanawake kama ilivyo kwa upande wa Wanaume ambapo kampeni hiyo itaambatana na shughuli mbalimbali za soka kuanzia asubuhi na itamalizika kwa kuchezwa mchezo mmoja Uwanja wa Sokoine  siku hiyo jioni baina ya timu za Wanawake za Mkoa wa Mbeya.

Mwenyekiti wa Soka la Wanawake Tanzania (TWFA), Amina Karuma akizungumzia kozi hiyo kwenda kufanyika Mbeya, amesema: “Tumetoka Lindi na sasa tunakwenda Mbeya, mpango huu utasaidia kuwajengea vijana wetu kujiamini hasa Wanawake.”

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mbeya (MREFA), Elias Mwanjala amewakaribisha washiriki watakaohudhuria kozi hiyo mkoani Mbeya akisema Mkoa huo upo tayari nkupokea ugeni huo kwa maendeleo ya mpira wa miguu.

Mpango wa Grass roots kabla ya kwenda kufanyika Mbeya ulifanyika huko Mkoani Lindi.

JPM atuma salamu za rambirambi kwa Spika kufuatia kifo cha mbunge
Godbless Lema amshukia mke wa Kafulila