Kiungo Mshambuliaji mpya wa Simba SC, Muivory Coast Aubin Kramo amesema kuwa amejiandaa vema kuleta ushindani katika msimu ujao ili awepo kwenye kikosi cha kwanza cha Mbrazili, Roberto Oliviera ‘Robertinho’.
Kramo ni kati ya wachezaji wapya wa kigeni waliosajiliwa na timu hiyo katika dirisha hili kubwa ambao wamekuja kuleta ushindani na kuipa makombe, kuipeleka hatua ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Muivory Coast huyo anatarajiwa kukutana na ushindani kutoka kwa Luis Miqquissone, Clatous Chama, Willy Onana na Kibu Denis katika msimu ujao.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Kramo amesema kuwa, ni kawaida kwenda katika timu mpya na kukutana na ushindani wa namba, kwake alilijiua hilo huku akijipanga kupambania namba mbele ya mastaa hao.
Kramo amesema kuwa, amesajiliwa na Simba kwa ajili ya kucheza, hivyo atahakikisha anatoa alichonancho kwa ajili ya kuisaidia timu hiyo, ili kufanikisha malengo ya msimu ujao.
Ameongeza kuwa haitakuwa kazi nyepesi kwake kuingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza, kutokana na ubora wa wachezaji waliosajiliwa ambao amewaona tangu siku ya kwanza aliyoanza mazoezi.
“Ni kawaida kwa kila klabu kubwa kuwa na wachezaji wazuri na ndio maana Simba ilifika Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Afrika, na mimi nimejiandaa kutoa nilichonacho kwa ajili ya kuisaidia timu yangu.
“Niupongeze uongozi kwa usajili bora ambao wameufanya katika dirisha hili kubwa, kikubwa kwa pamoja wachezaji tumekubaliana kufanikisha malengo ya timu ambayo ni kuchukua makombe.
“Kila mchezaji anapambana uwanjani kwa kutimiza majukumu yake atakayopewa na kocha ikiwemo kufunga, kuokoa na kutengeneza nafasi kwa wachezaji wenzetu,” amesema Kramo.