Kocha wa timu ya taifa ya Bulgaria Krasimir Balakov amekanusha taarifa za kuwepo kwa vitendo vya ubaguzi wa rangi, wakati wa mchezo wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Ulaya (Euro 2020) dhidi ya England, uliochezwa usiku wa kuamkia leo mjini Sofia.
Balakov amekanusha uwepo wa vitendo hivyo alipozungumza na waandishi wa habari mara baada ya mchezo huo, ambapo amesema hakusikia wala kuona mashabiki wakishiriki kwenye kadhia hiyo inayopigwa vita michezoni.
Amesema kilichotokea ni zogo la kawaida kutoka kwa mashabiki, ambalo mara kadhaa hutokea katika viwanja vya michezo, lakini sio kwa kisingizio cha ubaguzi wa rangi ambao umedaiwa ulikuwepo kwenye uwanja wa taifa wa Vasil Levski, ulioshuhudia wenyeji Bulgaria wakichabangwa mabao sita kwa sifuri.
“Binafsi sikuona wala kusikia vitendo vya kibaguzi, kilichotokea ni zogo la mashabiki ambao siku zote wamekua wakifanya hivyo kwenye viwanja vya michezo “, alisema Balakov
“Kama vilitokea vitendo kama hivyo vya ubaguzi wa rangi, huenda nilikua katika umakini wa kufuatilia timu yangu ilikuwa inapambana vipi uwanjani, lakini kusikia jambo kama hilo, sikulisikia kabisa.”
“Tulikua wengi uwanjani, huenda kila mmoja amesikia alichosikia, ila ninarudia tena kwangu sikusikia chochote kuhusu ubaguzi wa rangi ambao unadaiwa kufanywa dhidi ya wachezaji wa timu pinzani”.
Mabao ya England katika mchezo huo yalipachikwa wavuni na Raheem Sterling, Ross Barkley (mabao mawili kila mmoja) huku Marcus Rashford na Harry Kane wakifunga bao moja kila mmoja.