Waziri wa Kilimo, Profesa Adof Mkenda ametoa onyo kwa makampuni ya uzalishaji sukari kuwa serikali haitatoa vibali vya kuagiza sukari nje ya nchi ifikapo mwaka 2022 na kuvitaka viwanda hivyo kuongeza kasi ya uchakataji wa miwa ya wakulima na kuzalisha sukari ya kutosha.

Profesa Mkenda ametoa kauli hiyo leo Februari 15, 2021 wakati akiongea na uongozi wa Mkoa wa Morogoro akiwa ziarani kukagua hali ya uzalishaji sukari katika viwanda vilivyopo mkoani humo na pia kukutana na wakulima wadogo wa miwa.

“Shida yetu ya sukari haitokani na kukosa miwa bali ni uwezo mdogo wa viwanda kuchakata miwa yote ya wakulima nchini hali inayosababisha baadhi ya miwa ya wakulima kukosa soko,” amesema Waziri Mkenda.

Amebainisha kuwa Wizara ya Kilimo ina mkakati wa kuhakikisha miwa yote ya wakulima inachakatwa na viwanda vilivyopo ili kuondoa tatizo la upungufu wa sukari na kuwa utaratibu wa sasa viwanda kupewa vibali vya kuagiza sukari nje hauna manufaa kwa taifa.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emanuel Kalobero amesema Mkoa huo una viwanda vitatu vya kuzalisha sukari lakini bado uzalishaji wake ni mdogo hali inayopelekea miwa ya wakulima kukosa soko na kuharibika.

NHIF yakanusha kuondolewa huduma kwa wenye tatizo la upumuaji
Azam FC yatuma salamu Mbeya City