Siku moja baada ya Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Michezo na Sanaa kutangaza kulifungia gazeti la Mseto kwa kipindi cha miaka mitatu, Mbunge wa Ubungo ambaye pia ni mmoja wa Wakurugenzi wa Kampuni ya Hali Halisi inayotoa gazeti hilo, Saed Kubenea amenena.

Jana, Waziri Nape Nnauye alieleza kuwa wameamua kulifungia gazeti hilo kutokana na kuandika habari za uongo, kutumia nyaraka za kugushi pamoja na kumchafua Rais John Magufuli pamoja na Serikali kwa ujumla.

Hata hivyo, Kubenea ameeleza kupingana na uamuzi wa kulifungia gazeti hilo akidai kuwa ni mkakati ulioandaliwa dhidi ya vyombo vya habari nchini kwani hata hoja zilizotolewa wao hawakupewa nafasi ya kuzijibu.

“Hatukusikilizwa kutokana na hoja tuliyotakiwa kujibu ikiwemo ya kumchafua Rais Magufuli, huu ni mkakati kwa vyombo vya habari nchini,” Kubenea aliiambia Mtanzania.

Kubenea alieleza kushangazwa na kauli ya Serikali kuwa gazeti hilo limekuwa likionywa tangu mwaka 2012.

Mwanasiasa huyo machachari alisema kuwa Bodi ya Wakurugenzi wa Hali Halisi itakaa Jumapili hii na kuamua hatua watakazochukua dhidi ya uamuzi wa kufungiwa gazeti la Mseto.

Kigwangalla alitangazia kibano shirika la LGBT linalohamasisha Ushoga
Magufuli aapa kuirudisha CCM enzi za Mwalimu, wanachama kugawiwa mapato