Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es salaam,imefuta shtaka la uchochezi lililokuwa likimkabili Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), anayedaiwa kuandika makala iliyolenga kupotosha umma na kusababisha hofu kwa jamii.
Baada ya kulifuta shtaka hilo mshtakiwa alitoka nje lakini alikamatwa tena na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam, na kupelekwa Kituo cha Polisi kati ambako alihojiwa na baadaye kuachiwa kwa dhamana.
Kubenea alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Dereck Mukabatunzi mbele ya Hakimu Mkuu, Wilbard Mashauri kwa madai ya kuchapisha habari za uongo iliyolenga kusababisha hofu,taharuki kwa jamii na kuvuruga amani.
Hata hivyo, Hakimu Mashauri amesema kuwa hati ya mashtaka dhidi ya mshtakiwa ina mapungufu kwani kifungu cha 132 cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai (CPA), kinataka kosa hilo lielezwe kinagaubaga ni namna gani inapotosha jamii.