Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea jana alijisalimisha katika kituo kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kufutia tuhuma za uchochezi dhidi yake.

Kubenea anadaiwa kuandika makala ya uchochezi kwenye gazeti Mwana Halisi toleo la 349 la Julai 25-31 yenye kichwa cha habari, ‘Yuko wapi atakayeiokoa Zanzibar?’

Mbunge huyo ambaye pia ni mmoja kati ya wakurugenzi wa kampuni ya Hali Halisi inayochapisha gazeti hilo, alifika kituoni hapo majira ya mchana akiwa na mwanasheria wake, Tundu Lissu na alihojiwa kwa takribani saa mbili kabla ya kuachiwa kwa dhamana.

Baada ya mahojiano hayo, alisindikizwa na Jeshi la Polisi na kuzuiwa kuzungumza na waandishi wa habari lakini mwanasheria wake, Tundu Lissu alieleza kwa njia ya simu kuwa mteja wake aliachiwa kwa dhamana baada ya kuhojiwa kwa saa mbili kwa kile alichokiandika kwenye gazeti hilo.

“Kubenea amechiwa kwa dhamana na ameamriwa kurudi tena kituoni hapo tarehe 18 Agosti, mwaka huu,” Lissu anakaririwa.

Makala hiyo ya kubenea ilieleza kile alichodai amekishuhudia baada ya kusafiri hadi kisiwani Zanzibar, kuwa wananchi wananyanyaswa na kuteswa na Jeshi la polisi huku wengi wao wakibambikiwa kesi mbalimbali.

Lissu ambaye ni mtetezi wa Kubenea naye pia anakabiliwa na kesi za uchochezi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

 

Eneo la Ikulu lauzwa kinyamela
Maalim Seif agoma kumshika mkono Dk. Shein Msibani