Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea amefikishwa katika Mahakama ya wilaya ya Dodoma na kusomewa shitaka la kumshambulia Mbunge mwenzake Juliana Shonza wa CCM Julai 3 mwaka huu katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma
Akisoma shtaka linalomkabili Mbunge huyo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Dodoma James Karayemaha, wakili wa serikali, Beatrice Nsana amesema mtuhumiwa alitenda kosa hilo ambalo ni kinyume na kifungu 240 cha sheria ya makosa ya jinai sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Kubenea ambaye anatetewa na jopo mawakili watano wakiongozwa na Jeremia Mtobesya amekana kosa hilo na kuachiwa kwa dhamana huku upelelezi wa kesi hiyo ukiendelea na inatarajiwa kutajwa tena Julai 26 mwaka huu
Akizungumza nje ya ukumbi wa Mahakama Wakili Jeremia Mtobesya anasema ana imani na mahakama kuwa itatenda haki kwa mteja wake huku wenyekiti wa Chadema ambaye pia ni kiongozi wa Kambi ya upinzani bungeni akilaani kitendo hicho kwa madai kina lengo la kudhoofisha upinzani
Awali kabla ya Mbunge huyo kushtakiwa wabunge saba wa Chadema ambao ni Joseph Selasini,Pauline Gekul Cecilia Pareso,Frank Mwakajoka,Suzan Kiwanga,Devota Minja na kubenea juzi waliitwa na jeshi la polisi wakidaiwa kumshambulia Mhe Shonza.