Zikiwa zimesalia siku sita kabla ya Ligi Kuu soka Tanzania Bara kuendelea tena, Uongozi wa klabu ya Yanga bado unakuna kichwa ukifikiria mahali pa kuweka kambi ya muda mfupi.

Yanga itakuwa na kibarua kizito mwishoni mwa wiki ijayo itakapokumbana na African Sports ya Tanga maarufu kama Wana kimanumanu katika mchezo utakaopigwa kwenye uwanja wa Mkwakwani.

Wana kimanumanu ambao wanaonekana kuwa na hali mbaya katika Ligi Kuu msimu huu, huenda wakafanya lolote la kushangaza baada ya Jumamosi iliyopita kuonekana kuwa na mabadiliko kimchezo pale walipocheza mechi ya kirafiki na Azam FC na kutoka nao sare ya 1-1.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Klabu ya Yanga, Jerry Muro alisema bado uongozi unajadili mahali sahihi pa kupeleka timu ili iweke kambi.

“Hivi ninavyokwambia Yanga bado inaweka mambo sawa ili timu ikae kambini.Lengo letu ni kuhakikisha tunafanya vizuri katika Ligi pamoja na mashindano ya kimataifa,” alisema Muro.

Alisema mbali na suala la kambi pia Yanga lazima iongeze mchezaji katika kipindi hiki cha dirisha la usajili ili kujiimarisha.

“Yanga ni timu kubwa na siku zote huwa inafanya mambo yake tofauti na wale wenzetu wa mchangani”

Tangu Ligi itangazwe kusimama mwishoni mwa mwezi Oktoba, Yanga ilikuwa ikifanya mazoezi kwa kuhusisha wachezaji wa kikosi cha pili kifuatia wengine wengi kuwa katika timu ya Taifa.

TP Mazembe Kuifuata FC Barcelona Nchini Japan
Jose Mourinho Ajiondoa Nne Bora Msimu Wa 2015-06