Uchaguzi wa ubunge jimbo la Arusha Mjini umeahirishwa kutokana na kifo cha mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ACT-Wazalendo, Estomiah Mallah aliyefariki wakati akipewa matibabu katika hospitali ya rufaa ya KCMC.

Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Arusha, Juma Idd alieleza kuwa walizipokea taarifa za msiba huo kwa mshituko mkubwa hasa ikizingatiwa kuwa marehemu aliugua kwa muda mfupi sana.

Msimamizi huyo alieleza kuwa kufuatia msiba huo, walitoa taaria NEC na hivyo wamelazimika kuahirisha uchaguzi wa ubunge katika jimbo hilo kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi. Alifafanua kuwa wananchi jimboni hapo watapiga kura kuchagua rais na diwani pekee.

Akizungumzia mazingingira ya kifo cha mgombea huyo, Katibu wa ACT-Wazalendo jimboni humo, Eliaman Motivo, alisema kuwa wanayo masikitiko makubwa kufuatia msiba huo kwa kuwa wamempoteza mtu muhimu sana kwenye harakati za kizalendo za chama hicho na taifa kwa ujumla. Alisema marehemu alilalamikia hali ya afya yake kwa muda mfupi, lakini hali yake ilibadilika ghafla na kuwa mbaya kabla ya kupoteza maisha.

“Mzee alikuwa haumwi lakini kwenye mkutano wa mgombea urais wa chama chetu Oktoba 6, alipanda jukwaani na baada ya kushuka alisema hajisikii vizuri na kesho yake ambayo ni Oktoba 7, alikwenda hospitali ya St. Thomas na alipatiwa matibabu ila hali yake iliendelea kuwa mbaya. Tuliamua kumhamishia katika hospitali ya rufaa ya KCMC na usiku wa kuamkia jana alifariki, saa saba,” alisimulia.

Katika hali ya kusikitisha, katika kampeni za mwaka huu, wagombea watatu wa nafasi za ubunge wamepoteza maisha. Mgombea wa kwanza alikuwa Mohamed Mtoi wa Chadema, jimbo la Muheza, mgombea wa pili alikuwa mgombea wa CCM, Jimbo la Ulanga Mashariki, Bi. Celina Kombani.

Mungu awape faraja familia za marehemu hawa, wapumzike kwa amani. Amina!

 

 

 

 

 

Diamond, Vanessa Mdee Wang’ara Marekani Tuzo Za AFRIMA 2015
NEC Yaeleza Ukweli Wa Mashine Za ‘BVR’ Zilizokamatwa Dar