Hospitali ya Taifa Muhimbili imefunga mashine nne (Tatu Upanga na moja Mloganzila) za kujifukiza ambazo zimetengenezwa na SIDO ili kusaidia wagonjwa kupata tiba ya mfumo wa upumuaji kwa kutumia dawa za tiba asili zilizoidhinishwa na Serikali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru amesema wamefunga mashine hizo ili kuunga mkono jitihada za Serikali katika kukabiliana na magonjwa yanayohusiana na mfumo wa upumuaji ambapo gharama ya kujifukiza ni shilingi elfu tano kwa nusu saa.
“Wizara ya Afya ilielekeza kuimarishwa matumizi ya dawa za tiba asili kwa wagonjwa Hospitalini kama nyongeza kwenye tiba za kibingwa, Muhimbili imekuja na utaratibu wa kuwaruhusu wagonjwa kwa hiari yao kutumia dawa za tiba asili za kunywa na mvuke zilizoidhinishwa,” amesema Prof. Museru.
Aidha Prof. Museru ameeleza kuwa hatua hiyo ni moja ya njia za utafiti katika kukabiliana na janga jipya la virusi vya Corona ambalo bado halijapata ufumbuzi.
“Katika Hospitali zetu za Upanga na Mloganzila tuna Madaktari wa aina mbalimbali takribani 400, baadhi yao kupitia matumizi ya huduma hii ya tiba mvuke watafanya utafiti na kuwa katika nafasi ya kutuambia kama tiba hizi zinasaidia kwa kiasi gani, ugonjwa huu wa Covid 19 ni mpya hakuna aliye na majibu sahihi, kwa hiyo ni muhimu kwamba hizi njia zinazojitokeza, sisi tuliopo hapa tusizipuuzie bali tuzifanyie utafiti na kutoa majibu,” amesema Prof. Museru.
Mashine hizo zitaanza kutumika rasmi tarehe 05 Machi, 2021 kwa utaratibu maalumu ambapo wagonjwa watakaoruhusiwa ni wale watakaokubali kwa hiari yao wenyewe na wale wanaoweza kutembea na kusimama wenyewe kwenye mashine kwa muda usiozidi dakika tano.
Naye Mratibu wa Tiba Asili na Tiba Mbadala wa Mikoa na Wilaya kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Vumilia Liggyle amepongeza hatua ya Muhimbili kufunga mashine za kutoa tiba mvuke na ametoa wito kwa hospitali na taasisi nyingine nchini kuiga mfano wa huo ili kuendelea kupambana na magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.