Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni (WHO), limetaka suala la kukoma hedhi (Menopause), lijumuishwe katika huduma ya afya ya umma, kwa kuwa ni mwendelezo wa awamu ya afya kwa Mwanamke, kutokana na wengi wao kutotambua kile wanachopitia kama ni dalili za kuwa na tatizo hilo.
WHO imeyaeleza hayo kupitia ripoti yake iliyotolewa kwa vyombo vya Habari na kuongeza kuwa upo uwezekano kwamba wahudumu wa afya nao wanaweza wasiwe na uelewa wa dalili hizo huku Serikali nyingi nazo zikiwa hazina sera za afya na ufadhili wa kujumuisha uchunguzi wa changamoto za kukoma hedhi kwenye huduma za matibabu ya umma.
Aidha WHO imetaja dalili za tatizo hilo kuwa ni Joto la ghafla usoni, shingoni na kwenye kifua na kutoka jasho nyakati za usiku, kubadilika kwa mzunguko wa kawaida wa hedhi na hatimaye hedhi kukoma kabisa, ukavu sehemu za siri, maumivu wakati wa kujamiiana, kushindwa kushikilia haja ndogo na kubadili ghafla kwa mtazamo, shida ya kupata usingizi, kiwewe na msongo wa mawazo.
Hivi karibuni, Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na ajira duniani (ILO), lilianzisha mjadala wa iwapo suala la mwanamke kukata hedhi ni suala linalopaswa kuangaziwa pahala pa kazi, baada ya utafiti uliofanyika nchini Uingereza kubaini kuwa changamoto za kiafya zitokanazo na kukatika kwa hedhi zinasababisha wanawake wengi kutofanya kazi ipasavyo au kuacha kazi hali inayowaathiri kiuchumi.