Kitoweo cha samaki kinaelezwa kuwa na mafuta yenye kiambata aina ya Omega 3 yanayomfanya binadamu kuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri, kutunza kumbukumbu na kuishi kwa muda mrefu.

Vyakula vyote vinavyozalishwa majini huwa na kiambata aina ya Omega 3 yenye mafuta yanayotakiwa kwa mwili wa binadamu yatokanayo na samaki, yana mbegu maalumu zinazomsaidia binadamu katika ukuaji ambazo pia ni maalumu kwa faida ya mfumo wa ubongo na neva.

Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa watu wanaoishi maeneo ya pembezoni mwa bahari, maziwa, mito mikubwa wamekuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri, akili nyingi na wamekuwa wakiishi kwa muda mrefu kutokana na kutokuzeeka mapema.

Kwa upande wa Tanzania, watu waliozaliwa na kuishi maeneo ya pembezoni mwa bahari, maziwa, mito ikiwemo kisiwa kama cha Ukerewe na maeneo mengine karibu na maziwa Victoria, Nyasa, Rukwa hata visiwani Zanzibar wamebainika kuwa ni watu wenye akili nyingi na wanaishi kwa muda mrefu ukilinganisha na maeneo mengine ya nchi kitakwimu.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kituo cha Huduma ya Ushauri Nasaha, Lishe na Afya, Counselnuth, Mary Materu amethibitisha kuwapo na virutubisho vingi vinavyopatikana katika kitoweo hiki cha samaki iwapo wataliwa kwa wakati mwafaka mara tu baada ya kuvuliwa.

“Samaki wana kiambata aina ya Omega 3 ambayo husaidia katika ukuaji wa binadamu na kujenga ubongo wake vizuri, ndiyo maana watu wanaoishi katika maeneo yaliyozungukwa na maji mengi ‘bahari,  mito au maziwa’ ni watu wenye akili nyingi na watambuzi hata kama hajaenda shule na akienda shule hufanya vyema sana darasani kama ni mtoto, angalia watu wanaotoka ukerewe au sehemu nyinginezo,” amesema Materu.

“Wajawazito wanapaswa kula samaki kwa wingi ili kukuza ubongo wa mtoto, pia ni lazima wale nyama nyekundu ili kuongeza damu kwa uharaka mwilini ila tunawashauri isizidi nusu kilo kwa siku saba,”

“Omega 3 humsaidia mtoto kukuza ubongo, kutengeneza retina kwenye mboni ya macho na kutengeneza mfumo wa neva.

Pia, humsaidia mama kuzuia matatizo kama kifafa cha mimba na sonono baada ya kujifungua. Njia kuu ya mtoto kupata Omega 3 ni kutokana na vyakula anavyokula mama yake.

TANZIA: Prof Mwesiga Baregu afariki dunia
Rais Samia awasili Mwanza kwa ziara ya siku tatu