Scolastica Msewa – Pwani.
Zaidi ya Shilingi milioni 14. 7 na mifuko ya 880 ya saruji imepatikana katika harambee ya kukamilisha vyumba vitano vya madarasa na vyoo 26 katika Shule ya Msingi Kambarage, ikiwa ni Maadhimisho ya miaka 24 ya Kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu julius Nyerere Wilayani Kibaha, Pwani.
Harambee hiyo, iliyofanyika kwa ushiriano Taasisi ya kumbukumbu ya Mwalimu Julias Nyerere Mkoa wa Pwani na Uongozi wa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson John, Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Eng. Mshamu Munde ambapo Mgeni rasmi alikuwa Kaimu Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii – NSSF, Mkoa wa Pwani, Heri Abdi Kasingo.
Mbali ya kiasi hicho cha fedha kilichochangishwa, pia ilipatikana Dola za kimarekani 58, ahadi ya Madawati 50, nondo 62 na mchanga malori mawili huku Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Mkoa, John Kituka akiongoza Viongozi mbalimbali wa CCM ambapo zaidi ya shilingi milioni 2 ziliahidiwa na mifuko zaidi ya 300 ya saruji.
Katibu wa Taasisi ya kumbukumbu ya Mwalimu Julias Nyerere mkoa wa Pwani Omari Punzi alisema majukumu ya taasisi hiyo ni kushirikiana na Serikali kutafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson John amesema lengo la kufanya harambee hiyo ni kupata fedha ambazo zitasaidia kukamilisha vyumba hivyo vya madarasa na vyoo 26 ili hadi kufikia mwakani viwe vimekamilika.
Aidha Akizungumzia mahitaji ya vyumba vya madarasa Wilaya nzima ya Kibaha amesema anashukuru uongozi wa serikali ya awamu ya sita kwa jitihada kubwa za kujenga vyumba vya madarasa ambapo zaidi ya asilimia 90 ya mahitaji yamefanikishwa.
Diwani wa Kata ya Tumbi, Raymond Chokala ameshukuru kwa michango mbalimbali ya hali na mali ilikufanikisha ujenzi huo sambamba na kuwaalika Wadau mbalimbali wa Maendeleo kuendelea kuchangia miradi ya maendeleo katika Kata hiyo.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Kambarage, Happiness Msaki amesema kupitia harambee hiyo wamepunguza upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa na kuahidi kuongeza ufaulu kwa wanafunzi watakaomaliza darasa la saba mwakani.