Zikiwa zimebaki siku 27 watanzania wapige kura kumchagua rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wagombea urais wenye nguvu zaidi, Edward Lowassa (Chadema) na Dk John Magufuli (CCM) wameanza kukosoana kwa kutajana majina kwa mara ya kwanza.

Hapo awali, wagombea hao walikuwa wanawatumia zaidi wapambe wao kutaja majina na kukosoa lakini Dar24 imebaini matamko ambayo wawili hao wametajana.

Japokuwa mifano ya Magufuli ilikuwa inatoa uelekeo wa kuwa anamzungumzia Lowassa, hakuwahi kumtaja kwa jina isipokuwa juzi alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Busanda, Geita.

“CCM ni Malaika, ila kuna watu ambao si wazuri na wengine wameondoka, je, Lowassa, Sumaye, Mgeja, wote walikuwa CCM, sasa leo wanasema hakuna kilichofanyika, kama wameshindwa wakiwa katika nafasi ya uwaziri Mkuu, je wakipewa nchi,” alihoji Magufuli.

Kwa upande wa Lowassa, yeye pia alilitaja jina la Magufuli alipokuwa anawahutubia wananchi katika mkutano uliofanyika Mirirani alipowahoji wananchi kama kweli waliahidi kumpa kura mgombea huyo wa CCM.

“Nasikia alikuja Magufuli hapa mkasema mtampa kura zeni ni kweli?” Lowassa alihoji na kujibiwa ‘hapana’.

“Nipo Nyumbani, nina kila sababu ya kudeka. Nimefika kuwaomba kura zenu mtanipa? Wangapi wamejiandikisha hapa,” alisema.

Joto la uchaguzi linazidi kupanda huku wagombea hao wawili wakionekana kuwa na ushindani mkali kati ya wagombea nane wanaowania nafasi hiyo ya ngazi ya juu zaidi nchini.

Jana, Lowassa alipata mapokezi katika jimbo la Hai ambalo mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ndiye mbunge anayemalizina muda wake na anagombea nafasi hiyo tena. Wakati huohuo, Magufuli alikuwa akiendelea na kamepeni mkoani Shinyanga.

 

 

Magufuli Azua Taharuki, Achanganya Majina Ya Wasaliti Na Watiifu
Alichokisema Roma Baada Ya BASATA Kuufungia Rasmi Wimbo Wake ‘Viva’