Mchambuzi wa Michezo nchini Edo Kumwembe amewashukia baadhi ya Mashabiki wa Soka nchini kwa kuwataka kujenga misingi ya kuwaheshimu wachezaji ambao wamejitengenezea himaya katika Ligi Kuu na Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.
Kumwembe ambaye pia ni Mwandishi wa habari Mwandamizi ametoa rai hiyo kufutia kejeli zinazoendelea kwa Mshambuliaji na nahodha wa klabu ya Simba SC John Raphael Bocco ambaye msimu huu hajaanza vyema.
Akiwa kwenye kipindi cha Sports Arena cha Wasafi FM kilichorushwa leo Jumanne (Novemba 16) majira ya asubuhi Kumwembe amesema: “Kinachochekesha ni kwamba hata sasa ukiwaambia mashabiki wa Simba SC wanaomzomea Bocco kwamba amezeeka au amechoka basi aende Yanga, hakuna atakayekubali. Na hata wale wa Yanga ukiwaambia waletewe Bocco wote watashangilia. Huu ndio unafiki wa mashabiki wa Kitanzania.”
“Bocco anastahili heshima hata kama fomu yake ipo mbovu. Nadhani ni mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi katika historia ya Ligi Kuu. Amefunga mabao zaidi ya 100. Hata kama hayupo vizuri kwa sasa lakini tunahitaji kusimama nyuma na sio ‘kumuua’ zaidi.”
“Wenzetu huwa wanasimama nyuma ya mastaa wao ambao wanastahili heshima. Leo sio Bocco tu, hata Mbwana Samatta anatukanwa. Kisa? Kwa sababu Simon Msuva yupo katika fomu nzuri zaidi kwa sasa. Wanasahau mengi ambayo Samatta ameyafanya kuleta heshima ya nchi.”