Kundi la Haki za Binadamu limemuandikia barua Nicki Minaj likimtaka kuahirisha kushiriki tamasha lililoandaliwa na Mwana wa Mfalme wa Saudi Arabia, Mohammed Bin Salman maarufu kama MBS.
‘The Human Rights Foundation’ limemtaka rapa huyo wa kike kutoka Marekani kutohudhuria tamasha hilo liitwalo Jedah World Fest litakalofanyika Julai 18, 2019 na badala yake aungane nao kwakuwa wanaichukulia Serikali ya nchi hiyo kama Serikali inayokiuka haki za binadamu kwa kiwango cha juu.
Kupitia barua hiyo, wamemuomba arudishe fedha walizompa na atoe tamko la kulaani ukiukwaji wa haki za binadamu pamoja na kuitaka Serikali kuwaachia huru wanawake wanaharakati wa Saudi Arabia wanaoshikiliwa gerezani.
Aidha, kundi hilo limeeleza kuwa nchi hiyo haina uhuru wa vyombo vya habari na kwamba utawala wa Kifalme unadhibiti maudhui yote yanayorushwa kwenye vyombo vya habari.
Hatua hiyo inakuja wakati ambapo baadhi ya raia na makundi ya kidini ya Saudi Arabia yanalaani mualiko huo yakieleza kuwa uvaaji na picha chafu zilizoko mtandaoni zinazomuonesha rapa huyo ni kinyume na tamaduni na matakwa ya dini.
Baadhi wanaeleza kuwa tangazo la ujio wa Nicki ni hatari kwa malezi ya watoto na vijana waliolelewa katika maisha ya kidini kwani watajaribu kumtafuta kwenye mitandao na wataona picha zisizofaa; na huenda akawa sababu ya wao kuiga tabia isiyofaa.
Mwaka 2015, makundi ya Haki za Binadamu yalimtaka Nicki kutokubali mualiko wa kutumbuiza uliotolewa na Rais wa zamani wa Angola, José Eduardo dos Santos na kulipwa $2 million.
Hata hivyo, rapa huyo wa ‘Chun-Li’ alipuuzia wito huo na kupokea fedha za familia ya dos Santos ambazo wakosoaji wake waliziita ‘fedha za ufisadi’.
Lakini baadaye alieleza kuwa anajutia uamuzi wake wa na kwamba anadhani aliufanya wakati akiwa amelewa.
Bado Nicki hajatoa majibu yoyote kuhusu kushiriki au kutoshoriki tamasha hilo la Mwana wa Mfalme.