Serikali imewataka wananchi na taasisi ziache kuchapisha na kuziweka ofisini picha zisizo rasmi za Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Dk Philip Mpango na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa ameeleza hayo kwa waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya wiki ya serikali Mkoani mwanza ikielekeza picha zinatolewa na Idara ya Habari Maelezo nchini na zina alama maalum ya ulinzi na usalama.
Ametaja gharama ya picha hizo kwa atakayehitaji picha ya Rais Samia atalipia Sh15,000 huku ya Makamu wa Rais, Dk Mpango ikipatikana kwa Sh10,000.
“Hakikisheni mnakuwa na picha rasmi na mtu yoyote anayehitaji picha hizi zinapatika katika Idara ya Habari Maelezo Dodoma, Dar es Salaam na kwa wale ambao wanahitaji kutoka maeneo mengine tutawasiliana ili tuweze kukuletea picha ambayo ni rasmi,” amesema Msigwa.
Ameongeza kwamba picha ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na gharama yake itatambulishwa kwenye vikao vijavyo atakavyokuwa anavifanya kila wiki kwa mikoa tofauti.