Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA, John Mnyika amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anapaswa kuchukua hatua zaidi kwa waliotajwa katika ripoti ya CAG, na si kuvunja Bodi ya TRC pekee.
Mnyika ameyasema hayo wakati akiongea hii leo jijini Dar es Salaam na kusema Rais ana mamlaka makubwa kikatiba na kwamba hajayatumia kuchukua hatua juu ya waliobainika kufuja mali za umma na kusababisha hasara kwa Serikali.
Amesema, “hasara iliyosababishwa ni shilingi 503 Bililioni kwa kuchagua Mzabuni wa Trilioni 1.19 wakati kulikuwa na Mzabuni ambaye angeweza kufanya zabuni hiyohiyo ya ujenzi wa Reli kwa Tsh. Bilioni 616, hasara hii ina mnyororo mrefu, sio Bodi ya TRC pekee yake, mchakato wa kuingia mkataba wa malipo yaliyohusu Mzabuni huyu hayakuihusu Bodi pekee yake.”
Aidha, Mnyika ameongeza kuwa mchakato huo ulihusu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali lakini taarifa walizonazo zinasema idhini ya kufanya malipo ilifanywa na Wizara ya Fedha kwa barua ya Katibu Mkuu wa Hazina aliyekuwepo wakati huo, Dotto James kwa idhini ya Waziri wa Fedha aliyekuwepo wakati huo.