Shirikisho la soka nchini Tanzania (TFF) limewapa fursa mashabiki wengi kuingia uwanjani kuishangilia timu ya taifa ya wanawake wenye umri wa chini ya miaka 20 ‘Tanzanite’ itakayocheza na Falconets ya Nigeria, Jumapili Oktoba mosi, mwaka huu.

TFF imetoa ofa katika kiingilio.

Kiingilio kitakuwa ni Sh. 500 tu kwa mashabiki watakaoketi eneo la mzunguko huku kwa wale watakaokaa Jukwaa Kuu (VIP) watalipia Sh. 1,000 tu katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam.

“Lengo ni kuvutia mashabiki wengi wakaangalie soka la wanawake. Wakaingalie timu yetu. Wakaangalie uwezo wa timu yetu, waishangilie kwa nguvu zote,” amesema Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred.

Kocha wa Tanzanite, Sebastian Nkoma, amesema kwa namna alivyokiandaa kikosi chake ana imani kitaweza kupindua matokeo ya awali ambayo Tanzania kwa bahati mbaya ililala mabao 3-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Samuel Ogbemudian, ulioko Jimbo la Benin nchini Nigeria, wiki mbili zilizopita.

Issa Abdi Makamba atibiwa Dar
Jaji Manento aipongeza Serikali kwa kupitisha sheria upatikanaji wa taarifa