Mwanasiasa na aliyewahi kuwa Mbunge wa Kilwa Kusini, Seleman Bungala ‘Bwege’ amesema sifa moja ya Hayati Maalim Seif ilikuwa hataki kuona watu wafa ili yeye apate madaraka na ndio maana alikubali maridhiano na kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, nafasi ambayo haina nguvu na ni kama wapinzani walipakwa mafuta kwa mgongo wa Chupa.
Bungala aliyasema hayo hivi karibuni, wakati akifanya mahojiano maalum na Dar24 Media Nyumbani kwake jijini Dar es Salaam na kudai kuwa kitendo hicho kilipelekea watu kumuona Seif kama msaliti lakini alikuwa na uamuzi wenye wema ili kuepusha umwagaji damu, uamuzi ambao ulikuwa ni wa hekima.
“Nafasi ile haina nguvu kama ilivyo kwa Makamu wa pili wa Rais na yeye (Maalim Seif), si unaona watu wanajitokeza hadharani wanalalamika lakini wana nafasi kama wangelikuwa na nguvu wanalalamika nini, Maalim aliona mbali akaona ni bora niukose urais lakini watu wawe salama, watu walimuona na yeye ni kama CCM hapana haipo hivyo isipokuwa aliangalia mbali,” lalisema Bungala.
Aidha, Bwege amesema uwepo wake katika Siasa anauchukulia kawaida kwani anaamini watu wengi wanaishi maisha ya ya hali ya chini na kwamba usomi hauna matokeo chanya katika Taifa kwani utekelezaji wa mambo ya msingi hasa ya ya kimaendeleo ambayo yamekuwa yakisuasua hivyo kuifanya jamii iishi kwenye wakati mgumu.