Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Izack Njenga amesema ukosefu wa chakula katika nchi unaweza kuleta mandamano, kwani njaa huwa haina subira na hivyo kuhimiza uaandaaji wa mikakati katika kukabiliana na ukame.
Balozi Njenga ameyabainisha hayo wakati akifanya mahojiano maalum na Dar24 Media hivi karibuni na kutolea mfano ukame ulioikumba nchi ya Kenya, baada ya miongo minne kupita na kupelekea uwepo na tishio la baa la njaa huku akisema Mahindi ni zao muhimu na ni chakula kinacholiwa zaidi na watu wengi.
Amesema, “Ufaransa wananchi waliandamana kwa kulalamikia kupanda kwa gharama ya mkate na aliyekuwa malkia kwa kipindi hicho, Maria Antonent aliwahi kusema watu wanafanya maandamano kwa kukosa mkate kwanini wasile keki?, hakuja kama wamekosa mkate keki wangeitoa wapi.
“Kukiwa na upungufu wa chakula hata bei ya unga inaenda juu, na hiyo sasa inaleta upandaji wa gharama ya maisha na kuwa ndiyo kipimo cha kwanza hapo sasa tunarudi kunaangalia bei ya sukari, bei ya mafuta na mambo mengine yanafata,” amefafanua Balozi Njenga.
Aidha, ameongeza kuwa katika mipango ya Serikali bei ya mahindi ni lazima iangaliwe na kudhibitiwa kama ambavyo imekuwa ikifanya kwa kuweka ruzuku katika pembejeo za kilimo, kusudi iweze kuteremsha gharama za uzalishaji na kupunguza uwezekano wa athari zinazoweza kujitokeza iwapo bei ya unga itapanda.
Hata hivyo, amesema Kenya inahitaji zaidi zao la mahindi kutoka Tanzania kutokana na uzalishaji wake kuwa juu na kwamba wamekuwa na mipango na mikakati muhimu lakini miongo minne ya kiangazi iliwarudisha nyuma kwa miongo minne.