Uongozi wa Simba SC umetoa sababu za kupanga mchezo wao wa Mkondo wa Pili wa kuwania kufuzu Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Power Dynamos, kuchezwa majira ya saa kumi jioni.

Simba SC itakuwa mwenyeji wa mchezo huo utakaopigwa Jumapili (Oktoba Mosi) katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es salaam, huku akilenga kutinga hatua ya Makundi kwa mara ya tano tangu mwaka 2019.

Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema wameamua mhezo huo uchezwe saa kumi jioni, kutokana na michezo yao mingi msimu huu kuchezwa muda huo, hivyo itakua rahisi kwa wachezaji wao kupambana kwa mujibu wa mazingira walioyazoea.

“Mchezo dhidi ya Power Dynamos utachezwa siku ya Jumapili Oktoba mosi saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Azam Complex. Tumeamua kucheza saa 10 sababu michezo mingi hapa karibuni tumecheza muda huo hivyo hatukutaka kubadili muda lakini pia Jumatatu itakuwa siku ya kazi hivyo tunataka watu wawahi kurudi nyumbani.”

“Kuelekea kwenye mchezo huo ambao ndio utafatiliwa zaidi Afrika kwa wikiendi hii kutokana na matokeo ya mchezo wa kwanza. Ukubwa wa Simba SC ndio unafanya mchezo huo uwe mkubwa zaidi.” Amesema Ahmed Ally

Katika hatua nyingine Ahmed Ally amethibitisha kikosi chao kinaendelea na mazoezi ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Power Dynamos katika uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Amesema mazoezi yao yanafanyika uwanjani hapo ili kutoa nafasi kwa baadhi ya wachezaji wao wapya ambao hawajawahi kucheza katika Uwanja wa Azam Complex tangu waliposajiliwa mwanzoni mwa msimu huu 2023/24.

“Kikosi leo kimefanya mazoezi kwenye Uwanja wa Azam Complex pale Chamazi kwa ajili ya kuzoea uwanja. Tangu tumeanza msimu huu hatujawahi kutumia ule uwanja. Wapo wachezaji wetu wengi wanaujua uwanja ule na wapo wengine hawaujui.”

“Wachezaji watatu watakosekana kwenye huo mchezo. Wachezaji hao ni Aishi Manula, Henock Inonga na Aubin Kramo.” Amesema

Simba SC inahitaji matokeo ya sare isiyozidi 1-1 ama ushindi wowote ili kujihakikishia nafasi ya kutinga hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2023/24.

Henock Inonga kurudi mazoezini Simba SC
Usambazaji Umeme Vijijini kukamilika Desemba