Watu wengi hutegemea mifugo kupata riziki, Ufugaji wa wanyama humpa mfugaji nyama na maziwa kwa matumizi ya nyumbani na mapato kutokana na mauzo ya ziada, Mifugo pia ni chanzo cha samadi.
Mbuzi mara nyingi wanafahamika kama “Ng’ombe wa maskini” kwa sababu nyingi, Kwa yeyote anayetaka kufuga mbuzi kwa ajili ya maziwa, mbuzi anaweza kuwa rahisi kumhudumia kuliko ng’ombe.
Imeelezwa kuwa, Gharama za uanzishaji wa mradi wa mbuzi wa maziwa mmoja au hata watano ni ndogo ukilinganisha na kuanzisha mradi wa ng’ombe wa maziwa.
Chakula na zana za kufanyia kazi pia ni za gharama nafuu, Kufuga ng’ombe wa maziwa kunaweza kuwa changamoto kubwa kwa mtu anayeanza ufugaji, lakini kwa mbuzi ni sawa na kutafuta mnyama mwingine rafiki zaidi ya mbwa.
Mbuzi wa maziwa wanaweza kufugwa kwa gharama nafuu na kuishi katika mazingira magumu kama ya maradhi na ukame ikilinganishwa na ng’ombe.
Kutokana na umbile lao dogo wanaweza kufugwa katika eneo dogo na pia wanaweza kuhudumiwa na familia yenye nguvukazi na kipato kidogo, Uzao wa muda mfupi unamwezesha mfugaji kupata mbuzi wengi kwa kipindi kifupi.
Maziwa ya mbuzi ni mazuri kwa afya na yana ladha nzuri mno kuliko ya ng’ombe! Pia maziwa hayo yana protini nyingi kuliko maziwa ya ng’ombe. Ni mazuri kwa lishe, rahisi kunywewa na yana viinilishe vingi kwa sababu yana madini mengi ya kalsiumu, fosforasi na klorine kuliko maziwa ya ng’ombe.
Mbuzi anahitaji chakula kuanzia nusu tani hadi tani mbili kwa mwaka, kutegemeana na aina ya mbuzi, kiwango cha ubora wa chakula chenyewe, na mazingira mengine kwa ujumla.
Mbuzi pia anahitaji chakula cha nyongeza kama mahindi au mchanganyiko wa mahindi na ngano, pumba za nafaka na nafaka nyinginezo, Kwa kawaida, inategemea na nini kinacholimwa kwenye eneo husika au kinachopatikana. Mbuzi jike anahitaji chakula cha ziada ili kutoa maziwa mengi.