Katibu Mkuu mpya wa Chama Cha Wananchi (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa amesema chama hakina haja ya kuungwa mkono na wabunge wake ambao walikuwa upande wa Maalim Seif kwa kile alichokidai hata wakati wa mgogoro huo walikuwa hawaungwi mkono.
Amesema kuwa kwasasa wapo kwenye ujenzi wa chama chao hivyo hawahitaji tena migogoro na wako tayari kufanya kazi na Mbunge yeyote kama atakuwa tayari kuomba msamaha.
Aidha, amesema kuwa wao hawahitaji wabunge kiasi hicho, kwa sababu wakati wa mgogoro hawakuwasaidia kwa chochote, walikuwa wakiwatukana na kuwadhalilisha lakini amesema yameshaisha hivyo kazi kubwa kwasasa ni kujenga chama.
“Watu wenye mtihani mkubwa kwa sasa ni wabunge wa CUF, mimi nafikiri wanapaswa kuwa na busara sana, kwa upande wetu wabunge wametuumiza sana, wabunge wametumia pesa zao kutuumiza sana sisi tunaomuunga mkono Lipumba.” amesema Khalifa
Hata hivyo, mgogoro wa Chama Cha Wananchi (CUF) umedumu kwa zaidi ya miaka 3, mpaka pale Mahakama ilipotoa uamuzi kuwa Profesa Ibrahim Lipumba ndiye Mwenyekiti halali wa chama hicho na kupelekea aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif kuhamia ACT – Wazalendo