Mshambuliaji Alexis Sanchez amethibitisha kukabiliwa na majeraha ya kifundo cha mguu, akiwa kwenye kambi ya timu yake ya taifa inayoendelea kusaka nafasi ya kucheza fainali za kombe la dunia za 2018 kule nchini Urusi.

Sanchez ametoa taarifa za kuumia, kupitia akaunti yake ya mtandao wa Instagram.

Mshambuliaji huyo amepatwa na majeraha hayo ikiwa ni baada ya kushuhudiwa akirejea uwanjani juma moja lililopita, katika mchezo wa ligi ya nchini England dhidi ya Liverpool, ambapo kikosi cha Arsenal kilikubali kuchapwa bakora nne kwa sifuri.

Tukio hilo la kuumia pia linatokea, baada ya usajili wa Sanchez kuelekea Man city kukwama dakika za mwisho kabla ya dirisha la usajili halijafungwa Agosti 31.

Sanchez alikosa michezo ya mwanzoni mwa msimu huu, kufuatia maumivu ya misuli ya tumbo ambayo yalimuweka nje kwa muda wa majuma mawili.

Sanchez alihusishwa na mipango ya kutaka kusajiliwa na Man city kwa kitita cha Pauni milioni 60, huku nafasi yake ilitajwa huenda ingezajwa na mshambuliaji wa pembeni wa AS Monaco Thomas Lemar ambaye thamani yake ilifikia Pauni milioni 92.

Bado haijafahamika Sanchez atakuwa nje ya uwanja kwa kipindi gani, jambo ambalo huenda likaendelea kumuweka mashakani meneja wa Arsenal Arsene Wenger, ambaye anatamani kuendelea kumtumia, baada ya kugoma kumuuza.

Watanzania kubahatika Bima ya afya kwa 500
Ufaransa yabanwa mbavu na Luxembourg