Uongozi wa Mabingwa wa Soka nchini Ufaransa Paris Saint-Germain umempa ruhusa Mshambuliaji Kylian Mbappe kuzungumza na Al Hilal baada ya klabu hiyo ya Saudi Arabia kutuma ofa itakayoweka rekodi ya dunia ya Pauni Milioni 259.
PSG wamemuweka Mshambuliaji huyo sokoni na wamemuacha kwenye ziara ya timu hiyo kujiandaa na msimu mpya ya Korea Kusini na Japan na wameweka bayana kwamba wanataka kuwa na wachezaji ambao wana dhamira ya kuitumikia klabu yao.
Dau hilo nono la Al Hilal sio pekee PSG wamepokea, wamepata maombi mengi ya kumtaka nyota huyo kutoka klabu mbalimbali yakiwemo ya kutoa fedha na kubadilishana wachezaji, lakini miamba hiyo ya Saudi Arabia wameonesha dhamira kwa kuweka fedha nyingi itakayokwenda kuvunja rekodi ya dunia.
PSG wanaamini kuna klabu mpaka tano zinazomuwania Mbappe ikiwemo Tottenham.
Klabu nyingine zinazotajwa kumuwania nyota huyo ni Chelsea, Manchester United, Inter Milan na FC Barcelona.
PSG itasikiliza ofa yoyote ya kumtaka Mbappe na wamedhamiria kumuuza kwa fedha nyingi, ingawa klabu nyingine zitakuwa na wakati mgumu kufikia kiwango cha fedha kilichowekwa na Al Hilal.
Mbappe amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake na PSG na amegoma kusaini mkataba mpya, huku PSG ikiwa inaamini nahodha huyo wa Ufaransa tayari amefikia makubaliano ya kujiunga na Real Madrid kama mchezaji huru msimu ujao.