Beki wa Pembeni wa Mabingwa wa Soka nchini Ufaransa Paris Saint- Germain Achraf Hakimi anaamini Kylian Mbappe anastahili kushinda Tuzo ya Ballon dOr mbele ya Lionel Messi na Erling Haaland mwaka huu.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Morocco alimuunga mkono Mbappe kushinda tuzo binafsi yenye hadhi ya juu zaidi kwa mara ya kwanza, kufuatia mwanzo mzuri wa Mfaransa huyo msimu huu baada ya kuisaidia PSG kushinda mabao 2-0. dhidi ya Borussia Dortmund kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Akizungumza na belN Sports kutoa Ufaransa, Hakimi alisema: “Ukilinganisha na alichokifanya mwaka jana, kwangu, anastahili kushinda Ballon d’Or. Ni mchezaji mzuri na anaamini ataichukua mwaka huu.”
Messi kwa sasa ndiye anapewa nafasi kubwa ya kubeba tuzo hiyo baada ya kuisaidia Argentina kubeba ubingwa wa Kombe la Dunia Qatar mwaka jana.
Aidha wadau wengine wamempigia debe Haaland kutokana na mafanikio aliyopata kwa muda mfupi alipojiunga na Manchester City akitokea Dortmund.Haaland aliweka rekodi ya kufunga mabao 56 katika mechi 53 alizocheza na kuisaidia Man City kubeba mataji matatu likiwemo la Ligi Mabingwa Ulaya.
Mbappe alikosa ubingwa wa Kombe la Dunia lakini aliibuka kinara wa kufunga mabao manane na alifunga mabao 41 kwenye klabu yake msimu wa 2022-2023.