Mshambuliaji Kylian Mbappe hatahusika katika mechi ya ufunguzi ya Ligi Kuu Ufaransa maarufu Ligue 1, wakati Paris Saint-Germain itakapowakabili Lorient kesho Jumamosi (Agosti 12) kwenye Uwanja wa Parc des Prínces, kwa mujibu wa ESPN.

Mshindi huyo wa Kombe la Dunia mwaka 2018 hajafanya mazoezi na kikosi cha kwanza chini ya Kocha mpya, Luis Enrique huku kukiwa na mzozo wa mkataba na klabu hiyo.

Kwa mujibu wa vyanzo vya ESPN, Mbappe anaweza kukosa kila mechi ya PSG mwezi huu ambazo zitakuwa ni dhidi ya Lorient, Toulouse na Lens kama adhabu.

Mbappé hivi karibuni aliiambia PSG hataongeza mkataba wake na alipanga kuondoka katika klabu hiyo kwa uhamisho wa bure ifikapo Juni, mwakani.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa aliachwa katika ziara ya PSG ya Japan kabla ya msimu mpya, huku Rais wa Klabu hiyo, Nasser Al-Khelaifi akidai ama akubali mkataba mpya zaidi ya Juni-2024 au akubali kuondoka msimu huu wa joto.

Mshambuliaji huyo amefanya mazoezi na wachezaji (Wasiotakiwa) wakiwa njiani kuondoka PSG ambao ni pamoja na Leandro Paredes, Georginio Wijnaldum na Julian Draxler.

Al Hilal ndio klabu pekee iliyowasilisha ombi rasmi ila kutaka kumnunua Mbappé, lakini endapo atahama, anataka tu kujiunga na Real Madrid.

Madrid wamekuwa wakimfuatilia Mbappé kwa zaidi ya muongo mmoja na walijaribu kumsajili katika kila dirisha la uhamisho wa majira ya joto mawili yaliyopita.

Vyanzo vimeiambia ESPN vigogo hao wa Ufaransa, PSG iko tayari kutomchezesha Mbappé katika kikosi cha kwanza kwa msimu mzima kama mchezaji huyo hatabadili mawazo yake.

Mlinda Lango Azam FC akingiwa kifua
Try Again: Tunajipanga kwa Super League