Watahiniwa 1,397,370 wanatarajiwa kufanya Mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi hii leo Septemba 13 na 14, 2023 ambapo kati ya watahiniwa hao, 654,652 ni wavulana na wasichana ni 742,718 wakiwa na jumla ya masomo sita ya Kiswahili, Sayansi na Teknolojia, Hisabati, Lugha ya Kingereza, Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi na Uraia na Maadili.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania – NECTA, Dkt. Said Mohamed amewataka watahiniwa hao katika jumla ya shule 17,943 kuzingatia sheria na kujiepusha na vitendo vya udanganyifu na kudai kuwa Watahiniwa wenye mahitaji maalum ni 4,221 ambapo kati yao 101 ni wasioona.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania – NECTA, Dkt. Said Mohamed.

Amesema, pia 1,198 ni wenye uoni hafifu na 962 ni wenye uziwi, 487 ni wenye ulemavu wa akili na 1,473 ni wenye ulemavu wa viungo mwilini, huku akiwataka Walimu Wakuu, Waratibu Elimu Kata, Wamiliki wa shule, Wasimamizi wa Wakuu na wa Mkondo kutojihusisha na vitendo vya udanganyifu.

“Tunaamini kuwa Wanafunzi wameandaliwa vyema katika kipindi chote cha miaka saba, hatutegemei kuona watahiniwa wanafanya udanganyifu kwa kuwa tutawafutia matokeo. Si kitu tunachokipenda kuona mtoto amesoma miaka saba halafu anafutiwa matokeo,” alisisitiza Dkt. Said Mohamed.

Colombia yaongoza mauaji Wanaharakati wa Mazingira
Makubaliano ujenzi kituo cha Nyuklia yasainiwa