Mbunge wa Jimbo la Kawe kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Halima Mdee ameunga mkono agizo la Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango la kupiga mnada makontena 20 ya mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda.

Kupitia mtandao wake wa Twitter ameunga mkono agizo hilo huku akiwataka wananchi kujitokeza kununua samani hizo kama ambavyo Waziri Dkt.Mpango aliwataka watu wenye uwezo wa kununua wajitokeze bila kuogopa chochote.

“Wenye pesa zenu mnada ukipigwa jongeeni kwa wingi, laana ya kuku haiwezi mpata mwewe,” ameandika Mdee kwenye ukurasa wake wa Twitter

Aidha, Dkt. Philip Mpango, Agosti 27, 2018 aliagiza makontena 20 ya samani yaliyoingizwa nchini na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda yapigwe mnada ikiwa ni sehemu ya kusimamia sheria na kanuni za kodi zilizopo nchini.

Hata hivyo, tangazo la TRA lililotolewa na Kaimu Kamishna wa Forodha na Ushuru, Ben Asubisye lilikuwa na orodha ya makontena zaidi ya 800, huku jina la Paul Makonda lilijitokeza mara 20 akiwa mpokeaji wa makontena 20 yaliyopo katika bandari kavu ya (DICD).

Ujenzi wa barabara za juu umekamilika kwa asilimia 98- Majaliwa
Vitu 6 mwanaume wa kisasa anapaswa kuwa navyo