Lady Jay Dee ameeleza jinsi anavyomkumbuka msanii nguli wa Afrika, Oliver Mtukudzi maarufu pia kwa jina la ‘Jiwe la Afrika’, aliyefariki dunia jana mchana jijini Harare nchini Zimbabwe, chanzo kikiwa ni ugonjwa wa kisukari.
Mwimbaji huyo nguli nchini ambaye amewahi kufanya wimbo wa ‘Mimi ni Mimi’ aliomshirikisha Oliver Mtukudzi, amesema kuwa anamkumbuka zaidi kwa kubadili maisha yake ya muziki tangu alipomkimbilia na hatimaye kuzungumza naye walipokutana kwenye Tuzo za KORA nchini Afrika Kusini.
“Ni mtu ambaye amehamasisha (inspire) vizazi na vizazi Afrika. Na mimi namkumbuka nilikutana naye nilipotoa Albam yangu ya kwanza ya ‘Machozi’. Ilikuwa kwenye Tuzo za KORA nchini Afrika Kusini,” Lady Jay Dee aliiambia BBC.
“Ni mtu ambaye nilikuwa namuona ni mwanamuziki mkubwa na anafanya muziki mzuri. Kwahiyo nikamkimbilia nikamfuata na baada ya hapo maisha yangu yalibadilika, kwa sababu ushauri alionipa kuhusiana na mambo ya kufanya ‘Live Music’ na kuhusisha vionjo vya Kiafrika kwenye muziki, amehusika kwa kiasi kikubwa kubadilisha muziki wangu,” aliongeza.
Mtukudzi atakumbukwa kwa kuwa mwanamuziki nguli, raia wa Zimbabwe aliyeshiriki kikamilifu katika harakati za kutafuta uhuru wa nchi hiyo akitumia muziki wake.
Aidha, kutokana na kazi yake nzuri na mfululizo wa nyimbo zenye jumbe za kutetea haki za binadamu, alichaguliwa kuwa Balozi wa Mfuko wa Kimataifa wa Kuhudumia Watoto (UNICEF).
Alifanya jumla ya albam 59 zilizofanikiwa sana. Albam ya kwanza ni Ndipeiwo Zano aliyoiachia mwakaa 1978 na kuachiwa tena mwaka 2000, na ya mwisho ni han’a (Concern) ya mwaka 2018.
Amejinyakulia zaidi ya tuzo 25, zikiwa tuzo za muziki pamoja na tuzo za heshima alizopewa na mbalimbali ikiwa ni pamoja na mashirika ya umoja mataifa na Vyuo Vikuu.
Amefariki akiwa na umri wa miaka 66, ikiwa ni mwaka mmoja kamili tangu rafiki yake kipenzi, Hugh Masekela atangulie mbele za haki.