Watu 420,000 kati ya watu milioni 600 hufa Duniani, kwa kupata magonjwa yatokanayo na ulaji wa vyakula visivyo salama ambayo mara nyingi huwapata wenye kipato cha chini na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hii leo Juni 7, 2022 na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Nchini (TBS), Mhandisi Johaness Mganga kwenye siku ya Chakula Salama Duniani yenye kauli mbiu isemayo ‘Chakula salama afya bora’ imesema idadi hiyo inatokana na makadirio yaliyofanywa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
“Chakula kisicho salama husababisha magonjwa mengi na huchangia kurotesha afya ikiwemo udumavu, upungufu wa viini lishe na magonjwa mengine na hutokea zaidi kwa watu wenye kipato cha chini,” amesema Mhandisi Mganga.
Mhandisi Mganga kupitia tarifa yake amesema chakula salama huokoa maisha na kina mchango muhimu katika kupunguza magonjwa yatokanayo na kile kisicho salama ambapo uzalishaji wa chakula salama huongeza fursa za kiuchumi.
Amesema, kanuni bora za uzalishaji wa chakula salama huleta matokeo chanya, kupunguza uharibifu wa mazingira, upotevu wa chakula na kusisitiza uzingatiaji wa viwango stahiki ili kupata uhakika wa soko na kuondoa mdororo wa uchumi.
“Majukumu ya TBS ni kuhakikisha upo ubora wa chakula kinachoingizwa nchini na tumeweka mfumo wa udhibiti ili chakula kilichopo sokoni kiwe salama kwa kuilinda jamii dhidi ya madhara yatokanayo na chalula kisicho salama,” amesema Kaimu Mkurugrnzi huyo.
amesema magonjwa yatokanayo na chakula kisicho salama yanaweza kuzuilika iwapo kila mmoja atatekeleza wajibu wake na kwamba mlaji ana jukumu la uhakiki wa chakula anachotumia kuwa hakina madhara ya kiafya wakati wa matayarisho na kabla ya kukila.
Taarifa ya Kaimu Mkurugenzi wa TBS Mhandisi Mganga imesema maadhimisho ya siku ya chakula salama Duniani yanalenga kukumbusha jukumu la usalama wa chakula kwa wazalishaji, wasindikaji, wasafirishaji, wasambazaji, wauzaji, waandaaji na walaji.
“Lakini pia kauli mbiu hii inalenga kuonesha kuwa chakula salama ni muhimu katika kuimarisha afya na ustawi wa jamii maana manufaa ya chakula hupatikana pale tu kinapokuwa salama na TBS imejikita katika utoaji wa elimu kwa jamii na tumeandaa mkutano huu ili kuwasilisha ujumbe,” amesisitiza Kaimu Mkurugenzi huyo wa TBS.
TBS inasema Serikali imeweka mazingira wezeshi ya kutekeleza jukumu hili ikiwa ni pamo ja na kutunga sera, sheria, kanuni, kuweka viwango, miongozo mbalimbali, kutenga rasilimali za kutosha na kuboresha mazingira ya masoko na miundombinu.
Maadhimisho haya ya siku ya chakula salama Duniani yaliridhiwa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa uliofanyika Desemba 20, 2018 kwa azimio namba 73/250 ambapo siku ya kilele ni pale ifikapo Juni 7 kila mwaka.