Hatimaye Uongozi wa Klabu ya Young Africans umethibitisha kuachana na Beki kutoka nchini Ghana Lamine Moro, baada ya kuwepo kwa hali ya sintofahamu baina ya pande hizo mbili.
Moro aliingia matatizoni na benchi la ufundi la klabu hiyo chini ya Kocha Nasreddine Nabi, kwa kutajwa kama mkosa nidhamu, hali iliyopelekea kuondolewa kambini kwa majuma kadhaa kabla ya kurudishwa mwanzoni mwa mwezi huu.
Young Africans imetoa taarifa rasmi za kuachana na beki huyo aliyekua nahodha jana Jumatano (Julai 28), baada ya kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba uliokuwepo baina ya pande hizo mbili.
Hata hivyo taarifa za ndani zinaeleza kuwa hatua ya kusitisha mkataba wa beki huyo haitokani na kiwango chake, bali inaelezwa kuwa kitendo cha Lamine kutofautiana na kocha wa timu hiyo, Nesreddine Nabi pamoja na kuyumba kwa nidhamu yake hivi karibuni ndio kimepelekea kuvunjiwa mkataba, licha ya taarifa inayosambaa kutoeleza kadhia hiyo.
Inaelezwa kuwa katika makubaliano hayo ya kuvunjwa mkataba baina ya pande hizo mbili, Uongozi wa Young Africans umekubaliana kumlipa Lamine Moro mshahara wa mwezi mmoja.