Mwenyekiti wa kamati ya ufundi wa Yanga, Dominick Albinus, amesema wataendelea kukosa huduma ya mabeki wao muhimu Lamine Moro na Abdallah Shaibu ‘Ninja’.

Wawili hao walikosa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo FC uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita mjini Ruangwa mkoani Lindi, na kushuhduia timu hizo zikitoka sare ya bila kufungana.

Albinus amesema: “Kuhusu Lamine hayupo kwenye msafara wa timu yetu mchezo huu, amebaki pamoja na Ninja naye hatuko naye hivyo hawatakuwepo kwenye mchezo huu muhimu”

Katika hatua nyingine Dominic Albinius ‘Baba Paroko’ amesema kocha Nasrideen Nabi anapanga kusajili wachezaji wasiopungua watano katika safu ya ushambuliaji.

“Tunajua wapi pa kuanzia kwa msimu ujao na bahati nzuri ni kwamba kumleta kocha mapema (Nabi) kumeanza kuleta matunda kwa kocha kuanza kuonyesha anachotaka kwa msimu ujao.

“Mpaka sasa ripoti ya awali ambayo Nabi ametueleza anataka kuongeza mpaka wachezaji watano katika eneo la ushambuliaji na wengine kuwapisha wapya.”

Akifafanua zaidi Albinius amesema eneo hilo la ushambuliaji ndio litasimamiwa kwa umakini mkubwa ambapo washambuliaji wa kati mawinga na viungo wa pembeni wataongezwa.

“Kocha anasema timu inatengeneza nafasi shida ipo katika kuzitumia kwahiyo lazima tuongeze watu wenye ubora zaidi.

“Huku kwingine kwa viungo wa pembeni nako anataka mtu mwenye ubora zaidi, kwasasa kama tunamkosa Kisinda (Tuisila) hakuna nguvu nyingine pia anataka mtu eneo hilo,” amesema.

Aidha, alisema pia wanakusudia kutafuta kiungo mchezeshaji wa kati ambaye ataongeza ubunifu zaidi wa kutengeneza nafasi.

“Eneo la kiungo ushambuliaji wa kati nako kuna mtu anahitajika kocha anaona hakuna ubunifu wa kutengeneza nafasi nako tutatafuta mtu muafaka atakayekuwa na ubora wa kutengeneza nafasi eneo hilo.”

Waziri Bashungwa awaita mashabiki kwa Mkapa.
Bares apania alama tatu za Young Africans