Baada ya kuanza vizuri msimu mpya wa Ligi Kuu ya England (EPL) kwa kuibanjua Brighton & Hove Albion mabao matatu kwa moja, meneja wa Chelsea Frank James Lampard amekiri kufurahishwa na kiwango cha mlinda mlango wake kutoka Hispania Kepa Arrizabalaga.

Lampard ameonyesha furaha dhidi ya mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 25, kufuatia maneno mengi yanayoelekezwa kwa Kepa kufuatia kuonesha kiwango kibovu. Wachambuzi wa soka katika vyombo mbalimbali vya habari dunaini wamekua wakihoji nafasi ya kipa huyo kwenye kikosi cha Chelsea.

Mwishoni mwa msimu uliopita, Kepa alijikuta akimuachia Caballero nafasi yake na yeye kusugua benchi. Ni dhahiri mashabiki na wachambuzi wa soka walitarajia Chelsea wangesajili kipa mwingine katika dirisha hili la usajili, mpaka sasa usajili huo haujafanyika.

Akizungumza baada ya mchezo wao wa kwanza wa EPL Lampard amesema, “Ninafurahi kuwa na Kepa, kuhusu mkwaju ule, sidhani kama angefanya chochote cha ziada kuzuia asifungwe, lakini nimeona ameongeza kiwango cha kujiamini. Kepa yupo hapa na ni kipa wetu.”

“Kama tutasajili mwingine itakuwa ni ushindani tu. Hiyo ni asili ya Chelsea, ni kwa timu nzima, tutaona itakavyokuwa.”

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kusajili mchezaji mwingine, Lampard alijibu, “Hapana, sio kwa sasa. Bado tuna muda mpaka kufikia mwisho mwa dirisha hili la usajili.

“Tunakikosi kipana, tunapaswa kuangalia ni namna gani tunakiongoza tukitazamia ushindani ndani ya kikosi, kwa sasa hakuna habari yeyote kuhusu hilo.”

Ivory Coast: Mahakama yamuidhinisha Ouattara kugombea urais
IGP atoa maagizo ajali ya moto Kagera