Mshambuliaji wa Chelsea Tammy Abraham amefanyiwa vipimo vya afya, ili kufahamu kama ataweza kucheza mchezo wa ligi kuu ya England utakaowakutanisha dhidi ya Aston Villa, kesho Jumatano.
Meneja wa Chelsea Frank Lampard amethibitisha hatua ya kufanyiwa vipimo kwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 22, alipozungumza na waandishi wa habari mjini London leo mchana.
Abraham anaeongoza orodha ya wapachika mabao klabuni hapo kwa kufikisha mabao 11 msimu huu, alipatwa na majeraha katika mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Valencia uliomalizika kwa sare ya mabao mawili kwa mawili juma lililopita.
Hatua ya kuumia katika mpambano huo, ilimnyima nafasi Abraham kuwa kwenye kikosi mwishoni mwa juma lililopita, ambapo Chelsea walikubali kufungwa bao moja kwa sifuri dhidi ya West Ham United, huku nafasi yake ikichukuliwa na mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa Olivier Giroud.
“Tunatarajia kuwa na Abraham katika mchezo wa kesho, amefanyiwa vipimo na imeonekana amepona majeraha yake,” alisema Lampard kwenye mkutano na waandishi wa habari.
“Hatuwezi kuendelea kumuweka pembani, tunaamini atatusaidia katika harakati za kusaka alama tatu muhimu katika michezo ya ligi katika kipindi hiki cha mwezi Disemba.”
Katika hatua nyingine kiungo Ross Barkley ataukosa mchezo wa kesho dhidi ya Aston Villa, huku beki Antonio Rudiger akitarajiwa kurejea kikosini ndani ya siku kumi zijazo baada ya kupona majeraha ya nyonga.