Beki wa Arsenal Laurent Koscielny ataendelea kuwa nje ya uwanja hadi mwezi Disemba mwaka huu, kufuatia majeraha ya mfupa unaoshikilia kisigino, alioyapata wakati wa mchezo wa mkondo wa pili wa nusu fainali ya Europa League siku ya Al-khamis, dhidi ya Atletico Madrid.
Meneja wa Arsenal Arsene Wenger, amesema beki huyo kutoka nchini Ufaransa analazimika kufanyiwa upasuaji, ambao utamsababishiwa kuwa nje ya uwanja kwa kipindi cha miezi sita.
“Koscielny anahitaji kufanyiwa upasuaji, na itamchukua muda mrefu kurejea tena uwanjani,” Amesema Wenger akiwa katika mkutano na waandishi wa habari, kuelekea mchezo wa ligi ya England dhidi ya Leicester City.
“Tutarajie kumuona tena uwanjani mwanzoni mwa mwezi Disemba, akiwa katika uimara wake.”
Katika hatua nyingine kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ufaransa Didier Deschamps, tayari ameshamuondoa Koscielny katika mipango yake, kuelekea kwenye fainali za kombe la dunia, zitakazoanza Juni 14 nchini Urusi.
Wenger atakamilisha safari ya kukinoa kikosi cha Arsenal katika michezo miwili ya ligi iliyosalia msimu huu, akianza na mtanange wa kesho dhidi ya Leicester City na mwishoni mwa juma hili atapambana na Huddersfield Town.