Kocha Mkuu wa Chelsea, Mauricio Pochettino ameingiwa na hofu baada ya wachezaji wake muhimu kupata majeraha na atawakosa katika mechi ya mwishoni mwa juma hili dhidi ya Bournemouth.
Taarifa imeripotiwa kwamba staa mpya aliyesajiliwa, Romeo Lavia aliumia kifundo cha mguu wakati wa mazoezi wiki iliyopita huku Carney Chukwuemeka naye akipata majeraha.
Lavia hakujumuishwa kwenye kikosi tangu aliposajiliwa kwa Pauni 58 milioni kutoka Southampton ikidaiwa kwamba bado hakuwa fiti asilimia 100.
Pochettino aliweka wazi kwamba kiungo huyo atakuwa fiti baada ya mechi za kimataifa lakini sasa kutokana majeraha aliyopata huenda akaongezewa muda zaidi.
“Anahitaji muda wa juma moja zaidi kuwa fiti halafu atakuwa tayari kwa ajili ya mechi za ushindani. Anajaribu kujiweka fiti aungane na wachezaji wanzake. Tunatakiwa kusubiri.”
Wakati huo huo, Pochettino amepata pigo jingine baada ya nyota wake mwingine Chukwuemeka kuumia na huenda akawa nje ya dimba kwa muda mrefu.
Kwa mujibu taarifa, Chukwuemeka atakuwa nje kwa muda wa majuma sita baada ya kuumia katika mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya West Ham. Kiungo huyo alitarajiwa kurejea mwishoni mwa juma lijalo lakini sasa mambo yamekuwa tofauti.
Pochettino ameendelea kuwakosa Benoit Badiashile, Christopher Nkunku, Wesley Fofana ambao waliumia kabla ya msimu kuanza.
Lakini, Chelsea ilipata ahueni baada ya nahodha wa timu hiyo Reece James kusisitiza kwamba anaendelea vizuri kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii.