Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali itaendelea kukopa fedha kutoka taasisi mbalimbali, ili iweze kukamilisha miradi yake mbalimbali ya maendeleo inayoitekeleza.
Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) awamu ya tatu kipande cha kutoka Makutupora hadi Tabora, Rais Samia Suluhu Hassan amesema hakuna nchini duniani isiyokopa na kwamba hata nchi zilizoendelea zina mikopo mikubwa kuliko Tanzania.
Amesema kamwe Serikali haitavunjika moyo na haitarudi nyuma kutokana na kauli zinazotolewa na baadhi ya watu kuhusu suala la mikopo.
“Tutakopa tumalize miradi ya maendeleo ili tuendelee. Ukikopa unajenga sasa kwa haraka, ukisubiri ukusanye za kwako utamaliza lini kujenga? Mradi wa Matrilioni unasubiri za kwako utaumaliza lini,” Amesema Rais Samia.
Aidha Ameongeza kuwa Tanzania imekopa Mkopo wa Masharti nafuu wa miaka 20, unakudhuru nini? Maendeleo yanakuja haraka, utakusanya polepole uende ukalipe