Baada ya kumtambulisha Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Cameroon Leandre Willy Essomba Onana leo Jumatano (Julai 05) kupitia vyanzo vya habari vya Klabu ya Simba, Meneja wa Habari na Mawasilino wa klabu hiyo Ahmed Ally amefunguka mazito kuhusu mchezaji huyo.
Onana anakuwa mchezaji wa kwanza kutambulishwa Simba SC katika kipindi hiki cha kuelekea msimu mpya wa 2023/24, ambao unatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa kwa michuano ya ndani na nje ya Tanzania.
Ahmed Ally ametumia kurasa zake za Mitandao ya kijamii kufunguka kuhusu mchezaji huyo, ambaye amesajiliwa Simba SC akitokea Rayon Sports ya Rwanda, ambayo ilimaliza msimu uliopita ikiwa nafasi ya tatu, ikitanguliwa na APR iliyoibuka bingwa wa Ligi hiyo, ikifuatiwa na Kiyovu FC.
Ahmed Ally ameandika: Huu ndo usajili bora tangu dirisha la usajili lifunguliwe msimu huu nchini Tanzania
Mchezaji anatoka Taifa la mpira
Mchezaji amefunga magoli mengi
Mchezaji ana assist nyingi
Mchezaji ana tuzo nyingi
Mchezaji anatokea kulia, kushoto, katikati
Mchezaji huko alikotoka timu pinzani zimeshukuru kuondoka kwake maana alikua anawatesa
Mchezaji bado kijana na ana uwezo mkubwa
Mchezaji ana uwezo wa kuchezea mpira na kupiga mashuti ya mbali
???? ???????? ????????
Klabu ya Simba SC imemsajili Leandre Willy Essomba Onana kama mchezaji huru akitokea Klabu ya Rayon Sports ya Rwanda kwa Mkataba wa Miaka miwili.
Onana mwenye umri wa Miaka 23 Msimu uliopita alifanikiwa kuwa Mchezaji bora na Mfungaji bora wa Ligi Kuu Nchini Rwanda akifunga magoli 15 na kutoa asisti 10 kwenye Michezo 20 ya Ligi hiyo.
Anasifika kwa kasi, chenga na stamina akiwa na mpira, sifa ambazo zimekuwa zikimuwezesha kuwa kipenzi cha mashabiki wengi wa soka wanaomfuatilia huko nchi kwao Cameroon na hata nchini Rwanda alikotoka, pia anatarajiwa kuwa na wafuasi wengi katika ardhi ya Tanzania pindi tu atakapoanza kuitumikia Simba SC katika michezo ya Michuano ya msimu ujao 2023/24.
Vyanzo vyetu vya uhakika kutoka karibu na Mchezaji huyo vimeeleza kuwa, Simba SC imemsajili nyota huyo kwa dola za kimarekani 200,000 ambazo ni zaidi ya Shilingi Milioni 495 na huku akipokea Mshahara wa shilingi milioni 19 kwa Mwezi.