Uongozi wa klabu bingwa nchini England Leicester City una matumaini makubwa ya kufanikisha mpango wa kumuajiri aliyekua meneja wa muda wa Chelsea Guus Hiddink, baada ya kumtimua Claudio Ranieri mwishoni mwa juma lililopita.
Gazeti la The Guardian limeripoti kuwa, The Foxes wana matumaini hayo kutokana na mazungumzo ya awali dhidi ya meneja huyo kutoka nchini Uholanzi kwenda vizuri.
Gazeti hiyo limebainisha kuwa, sababu kubwa iliyowapa mwanya viongozi wa Leicester City kumfikiria Hiddink, ni kutokana na mafanikio ya muda mfupi ambayo aliwahi kuyapata akiwa na Chelsea kwa vipindi viwili tofauti.
Kutokana na hali waliyonayo Leicester City kwa sasa, wameona kuna haja ya kuelekeza macho yao kwa mtu huyo, kwa kuamini huenda kilichoisaidia Chelsea wakati wa utawala wake wa muda mfupi kitakua upande wao hadi mwishoni mwa msimu huu, ambapo wanapigania kutokushuka daraja.
Hata hivyo kuna tetesi zinazolezea kuwa, pamoja na kuwepo kwa mazungumzo mazuri kati ya uongozi wa Leicester City na Hiddink, huenda familia ya mzee huyo mwenye umri wa miaka 70 ikamzuia kufanya kazi kwa kushinikiza apumzike.
Hiddink aliwahi kueleza dhamira yake ya kustaafu ukufunzi wa soka wakati akiachana na Chelsea mwishoni mwa msimu uliopita, lakini mpaka sasa hajaeleza maazimio yake kama ameshaanza kuyafanyia kazi.