Mabingwa wa soka nchini England Leicester City wamefanikiwa kusonga mbele katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, baada ya kuifunga Sevilla CF kutoka Hispania mabao mawili kwa sifuri kwenye mchezo wa mkondo wa pili wa hatua ya 16 bora.
Wakicheza kwa mara ya kwanza michuano hiyo chini ya meneja wao wa muda Craig Shakespeare, Leicester City walitimiza azma hiyo kupitia kwa beki wao Wes Morgan na kiungo Marc Albrighton.
Hata hivyo Sevilla almanusura wapate bao kwa njia ya penati, lakini mpango huo ulishindikana kufuatia mlinda mlango wa Leicester City Kasper Schmeichel, kupangua mkwaju wa Steven Nzonzi.
Katika mchezo huo kiungo kutoka nchini Ufaransa ambaye anaitumikia Sevilla CF kwa mkopo akitokea Man City Samir Nasri, alioneshwa kadi nyekundu, ambayo ilitanguliwa na kadi mbili za njano.
Leicester City wanatinga katika hatua ya robo fainali kwa jumla ya mabao matatu kwa mawili.
Kama itakumbukwa vyema, mabingwa hao wa England, walipoteza mchezo wa mkondo wa kwanza katika uwanja wa ugenini huko nchini Hispania kwa kufungwa mabao mawili kwa moja.