Bao la kufutia machozi lililofungwa na mshambuliaji Jamie Vardy, limeiweka Leicester City katika mazingira ya kuendelea kuwa katika ushindani wa kusaka nafasi ya kutinga robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Sevilla CF.
Leicester City usiku wa kuamkia leo walikubali kufungwa ugenini mabao mawili kwa moja, matokeo ambayo bado yanashindwa kutoa mustakabali wa nani ataweza kusonga mbele kwenye hatua inayofuata kutoka na timu zote kuwa na nafasi.
Mabao ya Sevilla CF yalipachikwa wavuni na Pablo Sarabia na Joaquin Correa.
Hata hivyo Sevilla CF huenda wangeondoka na ushindi wa mabao matatu kwa moja, lakini mambo yalikua magumu kufuatia Joaquin Correa kukosa mkwaju wa penati.
Sevilla CF watalazimika kuulinda ushindi wao wa mabao mawili kwa moja watakapokua ugenini Machi 14 kwenye uwanja wa King Power nchini England.
Kwa upande wa Leicester City itawalamzimu kusaka ushindi wa bao moja kwa sifuri ama zaidi ili kujihakikishia nafasi ya kutinga robo fainali.
Wakati huo huo Mabingwa wa soka nchini Italia Juventus FC wamenza vyema kampeni ya kutinga hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya kwa kuichapa FC Porto mabao mawili kwa sifuri wakiwa ugenini mjini Porto-Ureno.
Mabao ya mabingwa hao wa Sirie A yalifungwa na mshambuliaji wa pembeni Marko Pjaca na beki wa kulia Daniel Alves katika dakika ya 70 na 72.
Timu hizo zitacheza mchezo wa mkondo wa pili mjini Turin nchini Italia Machi 14.